Jaji Mkuu awafunda viongozi wa Mahakama


Jaji Mkuu wa mahakama  aongea na viongozi wa Mahakama ,Serikali na viongozi wa Dini juu ya kuwaelimisha wananchi juu ya upatikanaji wa haki zao  Jaji Mkuu awafunda viongozi wa Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa wito kwa viongozi wa Mahakama, Serikali pamoja na Dini kuwaelimisha wananchi taratibu mbalimbali za upatikanaji wa haki.
Ameyasema hayo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na wakuu wa wilaya za Chemba na Kondoa, ambapo amesema kuwa wananchi wengi hawafahamu taratibu za upatikanaji wa haki hivyo viongozi hao wanao wajibu wa kuwaelimisha kwa lugha ya upole wanapofika kwenye maeneo yao ya kazi.
Amesema kuwa kutokana na kutokufahamu taratibu za upatikanaji wa haki, wananchi wengine wamejikuta wakipoteza haki zao na wengine kutumia muda mwingi kushughulika na kesi ambazo thamani yake hailingani na muda na mali iliyotumika.
“Wengine hudhani kupata haki ni kushinda kesi hawajui kwenye kesi kuna kushinda na kushindwa, dhana hii ndiyo inayoibua migogoro hivyo wananchi hawana budi kuelimishwa kuwa haki kwa aliyeshindwa ni kukata rufaa”, amesema Jaji Mkuu.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania imejiwekea vigezo ili kuhakikisha inaboresha huduma zake na wananchi wanapata haki kwa wakati.
Vigezo hivyo ni pamoja na kuhakikisha kesi inamalizika ndani ya miaka miwili kwenye Mahakama Kuu, miezi 12 kwenye Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja na Mahakama za Wilaya na miezi sita kwenye Mahakama za Mwanzo.
Aidha, ametaja kigezo kingine ni mapambano dhidi ya rushwa ambapo amesema kuwa Mahakama imesambaza nchi nzima mabango yenye ujumbe wa mapambano dhidi ya rushwa, simu za mikononi na pia imewapatia watumishi wake wote vitambulisho.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama pia hutoa nakala za hukumu bure na kuhakikisha nakala hizo zinatoka ndani ya siku 21, kupatikana kwa mienedo ya kesi ndani ya siku 30 ili kuwafikia wananchi na kutoa haki kwa wakati.
Naye Mkuu wa wilaya ya Chemba, Simon Odunga akimkaribisha Jaji Mkuu wilayani kwake amesema kuwa wilaya yake itaendeleza ushirikiano kati yake na Mahakama ya Tanzania.

Video: JPM apiga 8 nzito, Dkt. Bashiru uso kwa uso na Membe, Hujuma kubwa, Msajli ajibu hoja vyama 

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post