Kocha Msaidizi wa Simba SC Seleman Matola amefichua siri ya ushindi wa 4-2 dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana, katika Michuano ya maalum iliyoandaliwa na klabu ya Al Hilal ya Sudan.

Michuano hiyo iliyoanza mwishoni mwa juma lililopita katika Uwanja Al Hilal mjini Omdurman inashirikisha klabu za Simba SC (Tanzania), Asante Kotoko (Ghana) na wenyeji Al Hilal (Sudan).

Matola amesema kujituma na kufuata maelekezo kwa wachezaji wa Simba SC katika mchezo huo, ndio chanzo cha kupata ushindi huo chini ya Kocha Mkuu Zoran Maki.

Amesema baada ya Simba SC kutanguliwa kufungwa 1-0 dakika kumi za mwanzo, Kocha Mkuu Zoran Maki aliwahimiza wachezaji wake kutulia na kuelekeza mawazo yao mchezoni, na hatimaye walifanikiwa kusawazisha na kufunga mabao mengine mawili katika kipindi cha kwanza.

Simba SC iliongeza bao la nne kipindi cha pili huku Asante Kotoko walipata bao la pili katika kipindi hicho kwa njia ya Penati.

“Wachezaji walifanikiwa kufuata maelekezo ya Kocha, aliwahimiza watulie baada ya kufungwa bao la mapema, walifanya hivyo na kupanga mikakati mzuzi ambayo ilituwezesha kupata bao la kusawazisha na mabao mengine mawili katika kipindi cha kwanza.”