Watu wasiojulikana wamemmwagia mafuta yadhaniwayo kuwa ni Petroli kisha kumchoma moto na kumsababishia kifo Neema (Martha) Towo (30) Mkazi wa Kwa Mbonde, Kata ya Kwa Mathias, Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani ambaye ni Mhasibu wa BOA Bank Tawi la Kahama Mkoani Shinyanga.

  KKKT Usharika wa Tumbi ambako leo mwili wa Martha umeagwa kisha kusafirishwa hadi Moshi kwa maziko, ambapo Baba Mzazi wa Martha, Ndeonasia Towo amesimulia kilichomtokea Mwanae mbele ya Waombelezaji Kanisani.

Mzee Towo amesema Martha alifanyiwa kitendo hicho March 03,2023 saa 22:30 usiku, maeneo ya Mitamba Wilayani Kibaha ambapo Wahalifu hao walimpigia simu Martha akiwa Kanisani (KKKT Usharika wa Tumbi) na akatoka na kuwafuata kisha waliondoka nae na kwenda kumfanyia ukatili huo katika eneo hilo.

Mzee Towo anasema anaamini Martha hakuchomwa moto tu bali pia alichomwa dawa iliyoharibu figo zake lakini amesema Martha alikuwa jasiri maana hata baada ya tukio hilo alipambana na kukimbia akiwa ameungua hadi kwa nyumba za jirani na kuwatajia namba za Baba yake ili wampigie, baadaye Polisi walipewa taarifa na kumchukua Martha na kumpeleka Hospitali ya Tumbi kwa matibabu na baadaye alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uangalizi zaidi wa kimatibabu na alifariki usiku wa kuamkia Alhamisi March 09,2023.