Wafanyabiashara wanaoanza kutokulipa kodi kwa kipindi cha Miezi Sita au mwaka mmoja

 

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kibali cha kuruhusu wafanyabiashara wanaoanza biashara kutokulipa kodi kwa kipindi cha miezi sita hadi mwaka moja.

“Rais ametoa kibali, wale wanaoanza biashara kufanya biashara miezi sita hadi mwaka moja ndipo waanze kulipa kodi,” alisema. Alisema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Wilaya ya Kondoa.

Alisema hilo linaonesha ni jinsi gani Rais Samia anawajali wananchi wake. “Ni vyema kila mmoja akauunga mkono juhudi za Rais katika kuwaletea wananchi maendeleo,” alisisitiza. Pia aliwataka wananchi kuachana na mikopo umiza na ile ya kausha damu kwani imekuwa ikiumiza wananchi kutokana na kuwa na riba kubwa.

“Halmashauri zimekuwa zikitoa mikopo ya asilimia nne, wananchi mwende mkope huko. Pia Rais Samia ametoa fedha kwenye Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) ambapo mikopo hutolewa kwa riba ya asilimia tisa,” alisema. Alisema kuwa mikopo yenye riba kubwa imekuwa ikiumiza wananchi huku wakiwa hawapati faida yoyote.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post